Mtandao unaowasaidia wasichana kubaini iwapo uke wao ni wa kawaida


WasichanaHaki miliki ya pichaSCIENCE PHOTO LIBRARY
Image captionWasichana wengi wamekuwa hawaridhishwe na muonekano wa uke wao
Wasichana nchini Uingereza wanahimizwa kutumia huduma ya mtandaoni ili kuwasaidia kuangalia iwapo maumbile ya uke wao ni ya kawaida.
Huduma hiyo inapatikana kwenye mtandao wa masuala ya afya ya uzazi na ngono wa Brook, ambao unatoa mifano kwa kutumia video na kutoa ushauri kuhusu jinsi sehemu za siri za mwanamke hubadilika wakati anapobalehe au kuvunja ungo.
Lengo kuu ni kuwahamasisha wasichana kujikubali walivyo.
Watafiti wa afya waliotengeneza mtandao huo wamesema wana matumaini kwamba wasichana wataanza kujiamini zaidi na kuwafanya kutotaka ''upasuaji wa urembo'' wa sehemu zao siri.
Upasuaji wa aina hiyo haustahili kufanyiwa kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 18.
Upasuaji huo wa urembo wa sehemu nyeti maarufu kama- labiaplasty - unaofanywa kuongeza au kupunguza sehemu hizo hutekelezwa na madaktari binafsi ambao hutoza maelfu ya mapauni.
Kwa mara nyingi, operesheni hiyo huweza kufanywa na mamlaka ya huduma ya afya -NHS iwapo sehemu nyeti za msichana zina kasoro, iwapo inamsumbua au inamwathiri kiafya.
Madaktari wa afya hawastahili kutoa uamuzi kwamba wasichana wafanyiwe upasuaji kwa sababu ya urembo pekee.
Kulingana na takwimu za NHS, 2015-16 zaidi ya wasichana 200 chini ya miaka 18 walifanyiwa upasuaji wa sehemu zao za siri na zaidi ya 150 ya wasichana hao walikuwa chini ya miaka 15.
Picha ya sehemu za siriHaki miliki ya pichaBRITSPAG
Image captionPicha ya sehemu za siri
Bi Louise Williams, ambaye ni muuguzi katika chuo kikuu cha University College Hospital na kiongozi wa mradi huu, amesema: "Elimu hii itawasaidia wasichana kuelewa sehemu zao za siri na jinsi inavyokomaa wakati wanapovunja ungo, haswa wakiwa na wasiwasi jinsi wanavyojitizama au kijihisi.
"Tuna matumaini kwamba tutawahakikishia wasichana kwamba sehemu zao za siri ziko na maumbo tofauti na ukubwa fulani na iwapo wanahitaji usaidizi na mawaidha , wanaweza kujua pale watakapopata ujumbe huu.''
Dkt Naomi Crouch kutoka chuo cha taasisi cha Royal College cha Madaktari wa uzazi na wataalamu wa afya ya uzazi na shirika la Uingereza la watoto pia walihusika kwenye utafiti huo.
Alisema: "Hakuna utafiti wowote wa kisayansi ambao unaounga mkono upasuaji wa sehemu za siri na iwapo una athari zozote za kimwili au kisaikolojia hasa kwa vijana ambao bado wanakuwa.
"Tunatumai kwamba ujumbe huu utawapatia wasichana ufahamu zaidi kwa kwamba sehemu zao za siri ni maalumu na hubadilika wanapokua maishani na ni kawaida."

Upasuaji kwenye uke unaweza kusababisha madhara

Upasuaji huo unaweza kusababisha:
  • Uvujaji wa damu
  • Maambukizi
  • Uharibifu wa tishu za mwili
  • Kupunguza hisia za sehemu hizo za siri
Kunaweza kuwa na matatizo mengine madogo:
  • Kuganda kwa damu kwenye mishipa
  • Kuathirika na dawa za kulala unapofanyiwa upasuaji.

Comments